Tuesday, 4 June 2013

Liewig: Simba msinitanie, nasubiri tiketi ya kuja Dar


PATRICK Liewig yuko pale Paris akisubiri tiketi ya ndege kutoka kwa Zakaria Hanspope ili arudi Dar es Salaam haraka kuiandaa Simba kwa Kombe la Kagame linaloanza baadaye mwezi huu nchini Sudan.
Lakini aliposikia Simba yake imeanza mazoezi tangu Jumanne kwenye Uwanja wa Kinesi pale Shekilango, Dar es Salaam chini ya Kocha mpya Abdallah Kibadeni akashtuka kidogo aangushe simu. Halafu baadaye akacheka na kuuliza hivi: “Hivi unaniambia kweli au unanitania?”.
Liewig amesema Hanspope ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili wa Simba amemuhakikishia atamtumia tiketi na wamekubaliana mambo mengi wakati anaondoka na hajaambiwa kwamba kazi yake imeota mbaya.
“Ni kitu cha ajabu sana kama Simba itakuwa imeanza mazoezi na kocha mwingine wakati mimi nina mkataba nao mpaka Juni, halafu sijaambiwa lolote. Mimi nimekaa nao mpaka naondoka wameniambia kazi yangu iko salama na Hanspope akaniambia nisubiri tiketi muda wowote,”alisema Liewig mwenye umri wa miaka 62 na ambaye Mwanaspoti linajua kwamba barua yake ya kufukuzwa ipo tayari na atatumiwa leo Jumamosi kwa njia ya barua pepe (email).
“Ninasubiri taarifa rasmi ya uongozi kwavile sijafukuzwa, mimi bado ni kocha wa Simba. Nimefanya kazi kwenye mazingira magumu sana kuna kipindi nilikuwa sina hata usafiri, mishahara ilikuwa inachelewa lakini kwavile mimi ni profeshno nikawa naficha siri na nafanya kazi yangu kwa heshima ya Simba.
“Lakini kama wameanza mazoezi bila mimi kuwepo si utaratibu na haikubaliki popote pale Duniani, hawawezi kuendesha mambo hivyo lazima tubadilike twende kiprofeshno hata huyo kocha aliyeajiriwa na mwenyewe anafanya makosa.
“Nilikuwa na mambo mengi sana nimeyaacha mezani juu ya uendeshaji wa timu na mpangilio wa benchi la ufundi na usajili tayari kwa msimu mpya na hayo yote yamezingatia hali ya uchumi ya Simba sasa sielewi hizo ripoti unazonipa kwamba Simba iko mazoezini bila mimi, sielewi,”alisisitiza kocha huyo.
Makamu Mwenyekiti wa Simba, Joseph Itang’are ‘Mzee Kinesi’ amethibitisha kwamba Liewig si kocha wao na wala hawana mpango naye tena na ndio maana Kibadeni na Jamhuri Kihwelu ‘Julio’ wamepewa timu.
(source: mwanaspoti.)

No comments:

Post a Comment