
Evans Aveva ametaja sababu kadhaa za timu hiyo kufanya vibaya msimu huu, mojawapo ni kuwa na wachezaji wasio waaminifu baadhi yao beki Hassan Kessy na mshambuliaji Ibrahim Ajib
Rais wa Simba SC, Evans Aveva ametaja sababu kadhaa za timu hiyo kufanya vibaya msimu huu, mojawapo ni kuwa na wachezaji wasio waaminifu baadhi yao beki Hassan Kessy na mshambuliaji Ibrahim Ajib.
Akizungumza katika Mkutano na Waandishi wa Habari Jumanne katika Hoteli ya Collessium, Barabara ya Nyerere, Dar es Salaam, Aveva alisema wachezaji hao walifanya vitendo ambavyo vimewaondolea uaminifu katika klabu.
Aveva alisema Kessy alitolewa kwa kadi nyekundu katika mchezo wa Ligi Kuu na baada ya adhabu hiyo, klabu ikaamua kumuongezea adhabu, lakini kabla hajamaliza adhabu zake akaibuka kusaini kwa mahasimu Yanga
Kuhusu Ajib, Aveva alisema mshambuliaji huyo alitolewa kwa kadi nyekundu katika mchezo wa Ligi Kuu pia na asubuhi yake akapanda ndege kwenda Afrika Kusini.
Amesema mambo kama hayo pamoja na uendeshwaji mbovu wa Ligi Kuu unaofanywa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) vimechangia Simba SC kufanya vibaya msimu huu.
Aveva amesema kutakuwa na Mkutano Mkuu wa klabu Julai 10, mwaka huu kujadili matatizo ya klabu na kutafuta suluhisho lake.
Kauli ya Aveva inakuja baada ya Ibrahim Ajib kufuzu majaribio katika klabu ya Lamontville Golden Arrows FC ya Ligi Kuu ya ABSA Afrika Kusini.
Hata hivyo, klabu hiyo haiko tayari kumnunua mchezaji huyo bali inataka kumchukua kama mchezaji huru na kumsainisha mkataba.
Kwa sababu hiyo, klabu hiyo imemtaka Ajib kurejea klabuni mwake kuangalia kama Mkataba wake umekwisha apeleke uthibitisho Afrika Kusini ili apewe Mkataba Arrows.
Wakala wa mchezaji huyo, Juma Ndabila ameliambia Lete Raha kwamba wanarejea Dar pamoja na Ibrahim Ajib.
“Amefuzu majaribio, lakini kuna suala la mkataba hapa, yeye alisema kamaliza mkataba, na Simba wanasema bado ana mkataba, kwa hivyo anarudi kutatua hilo suala,” amesema Ndabila.
Kwa upande wake, wakala aliyemuunganishia majaribio Ajib Afrika Kusini, Rodgers Mathaba amesema kwamba mchezaji huyo amepewa fursa ya kurudi Arrow wakati wowote akiwa mchezaji huru.
“Amefuzu majaribio, sasa ni juu yake anatakiwa hapa kama mchezaji huru, anarudi Dar es Salaam kushughulikia mkataba wake, nafasi yake ipo wazi hapa wakati wowote,” amesema Mathaba.
No comments:
Post a Comment